European External Action Service

08/27/2026 | News release | Archived content

Mwanzo wa Usalama wa Chakula: Hadithi ya Shamba Moja la Ukraine

Kituo cha kisasa cha kukamulia, ambacho hapo awali kilikuwa kitovu cha shughuli za kila siku za shamba, kilikuwa kimeharibika kabisa. Mashamba yaliyopaswa kutayarishwa kwa ajili ya kupanda ngano, mahindi na alizeti hayakuwa salama - mabomu ya ardhini na makombora ambayo hayakuwa yamelipuka yalikuwa yametapakaa kote, na kufanya isiwezekane kuingia humo kwa usalama.

Shamba lake la Naporivske katika kijiji cha Lukashivka lilikuwa chini ya uvamizi wa jeshi la Urusi kwa takriban mwezi mmoja. Wanajeshi wa Urusi waliliteka katika wiki za mwanzo za uvamizi kamili. Eneo hilo lilishambuliwa kwa makombora, na baadaye Hryhorii alisema kuwa takribani makombora 60 yalianguka kijijini na kwenye shamba lake. Kufikia wakati majeshi ya Ukraine yalipowafurusha wanajeshi wa Urusi mwishoni mwa Machi 2022, hakukuwa na jengo hata moja katika shamba hilo ambalo halikuwa limeathiriwa.

Kwa Hryhorii, hii haikuwa tu hasara ya kibiashara. Yeye, mke wake na watoto wao wanne walikuwa wamejenga shamba hilo kwa miaka mingi, wakilianzisha kutoka shamba ndogo la kifamilia hadi kuwa mmoja wa waajiri wakubwa zaidi katika eneo hilo. Walianza na ng'ombe wachache, hekta kadhaa za ardhi, bila vifaa vya kutosha na wakiwa na mtaji mdogo sana wa kuanzia. Kazi nyingi za mwanzo zilifanywa kwa mikono. Kadiri muda ulivyopita, shamba hilo lilikua na kuwa biashara ya kisasa ya kilimo yenye takribani hekta 1,500 za ardhi, mamia ya ng'ombe, uzalishaji wa mazao na maziwa, pamoja na wafanyakazi wengi.

Katika wiki za kwanza za uvamizi, Hryhorii na timu yake waliendelea kukamua ng'ombe kadri walivyoweza, hata walipokuwa wakikabiliwa na tishio la mashambulizi ya makombora. Kiwanda cha kuchakata maziwa hakikuweza tena kuyakusanya maziwa kutokana na mashambulizi ya mabomu, hivyo shamba hilo lilisambaza maziwa kwa vijiji vya karibu. Sehemu ya maziwa hayo ilipelekwa na Shirika la Msalaba Mwekundu kwenye vituo vya kulelea watoto yatima na hospitali. Hata walipokuwa wakishambuliwa, shamba hilo liliendelea kujitahidi kulisha watu.

Kisha jeshi la Urusi liliteka shamba hilo.

Hryhorii aliporudi mwezi mmoja baadaye, baada ya jeshi la Ukraine kukomboa kijiji hicho, alikuta zaidi ya ng'ombe na ndama wake 100 wameuawa. Baadhi walikufa wakati wa mashambulizi ya mabomu; huku wengine, kwa mujibu wake, wakipigwa risasi. Ndama walibaki bila mama zao. Mizoga ya wanyama ilikuwa imetapakaa kote shambani.

"Warusi walichinja karibu nusu ya ng'ombe wangu na kuwafanya nyama ya kebabu ambayo waliichoma kwenye kanisa la kijiji," aliambia The Telegraph. "Walikuwa kana kwamba wako kwenye safari ya kuwinda,"alisema, akielezea kupigwa risasi kwa wanyama hao kama kitendo cha ukatili badala ya ulazima.

Ufugaji wa ng'ombe wa maziwa unategemea utaratibu na uangalizi wa kila siku: kuwalisha, kuwakamua, kusafisha mazizi, kuwapa matibabu, kuzalisha mifugo, na kuwahudumia kwa karibu na watu wanaowafahamu vizuri. Kwa hivyo, kuchinjwa kwa ng'ombe hao hakukuwa tu pigo la kiuchumi-kuliharibu mfumo hai wa uzalishaji uliokuwa umejengwa kwa miaka mingi. Hali hiyo ilimwachia Hryhorii na timu yake kazi ngumu lakini zisizoepukika: kuondoa mizoga ya wanyama, kukagua majengo yaliyoharibiwa, kuwatafuta wanyama walionusurika, kutengeneza walichoweza kutengeneza, na kutathmini kama mashamba yangeweza kutumika tena.

Hakukuwa na muda mwingi wa kuomboleza; msimu wa upandaji wa masika ulipaswa kuanza. Lakini mashamba yalikuwa hatari, mafuta yalikuwa haba, vifaa vilikuwa vimeharibika, maghala ya mbolea yalikuwa yameshambuliwa, na kingo za barabara zilikuwa zimetapakaa mabomu na vilipuzi ambavyo havikuwa vimelipuka. Mabomu ya ardhini na vichwa vya makombora ambavyo bado vilikuwa hai vilipaswa kutafutwa na kuondolewa kabla ya mashine kuweza kufanya kazi kwa usalama mashambani.

Mwanzoni, Hryhorii alisema hakuweza hata kufikiria aanzie wapi. Kisha uhalisia wa hali hiyo ukawa jambo ambalo hangeweza kuliepuka. Wanyama walionusurika walihitaji kutunzwa huku mashamba yakihitaji kupandwa. Wafanyakazi walihitaji ajira, ilhali vijiji vilikuwa vinakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Kujenga upya hakukuwa kauli mbiu; kulikuwa ni orodha ndefu ya kazi za kuchosha.

"Ninatambua kuwa kuna watu wengi wanaotegemea kufanya kazi hapa, na sharti nihakikishe kuwa shughuli zinaendelea," alisema.

Kilichotokea katika shamba la Naporivske hakikuwa na athari kwa kijiji hicho pekee. Mashamba kama la Hryhorii yanapoharibiwa, athari zake huenea mbali zaidi ya kijiji kimoja. Usambazaji wa maziwa husimama, mashamba hubaki bila kupandwa, na chakula ambacho kingelisha watu duniani kote hakitoki tena shambani. Mnamo Machi 2022, wakati vita vya Urusi vilipovuruga shughuli za kilimo na mauzo ya bidhaa kupitia eneo la Bahari Nyeusi, bei za chakula duniani zilifikia viwango vya juu zaidi kuwahi kurekodiwa. Baadaye, Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa uliwezesha kusafirishwa kwa karibu tani milioni 33 za nafaka na vyakula vingine kutoka bandari za Ukraine kwenda katika nchi 45-kumbusho kwamba mifumo ya usalama wa chakula iliyo mbali nje ya mipaka ya Ukraine inategemea mashamba yake.

Usalama wa chakula huanzia kwenye shamba la kila mkulima. Hautegemei tu makubaliano ya kimataifa bali, kwa upande wa Ukraine, unategemea pia mambo kadhaa muhimu. Mkulima sharti aweze kuingia kwenye shamba lake kwa usalama. Ng'ombe wa maziwa wanapaswa kubaki hai. Kikaushio cha nafaka kinapaswa kuendelea kufanya kazi. Wafanyakazi wanapaswa kubaki kijijini. Barabara na maghala ya kuhifadhi mazao yanapaswa kufanya kazi ipasavyo. Na mwishowe, biashara ya kifamilia lazima iweze kustahimili hasara ambazo zinaweza kuzifilisisha biashara nyingi.

Shamba la Naporivske limeanza kurejea polepole katika shughuli zake. Mashamba yake yanalimwa tena. Shamba hilo limefanikiwa kurejesha sehemu ya mifugo yake. Vita hiyo pia ililazimisha mabadiliko; shamba hilo lilianza kujihusisha na uchakataji wa maziwa, ikiwemo utengenezaji wa jibini.

Huenda shamba hilo likarejea kwenye shughuli za kawaida, lakini makovu ya uharibifu wake bado yapo. Hryhorii anaendelea kuhifadhi kumbukumbu za yaliyotokea: mabaki ya risasi na silaha zilizotumika kushambulia eneo hilo, vifaa vilivyoharibiwa, pamoja na kumbukumbu za wanyama waliouawa na majengo yaliyobomolewa.

Hadithi yake si simulizi la ustahimilivu wa kihisia tu. Ni hadithi kuhusu uwajibikaji. Alirejea kwa sababu kulikuwa na kazi iliyopaswa kufanywa, kwa sababu watu walitegemea shamba hilo, na kwa sababu ardhi haiwezi kujijenga yenyewe. Athari za vita hivyo kwa dunia zinaweza kupimwa kwa kupanda kwa bei, mauzo ya bidhaa nje ya nchi na mamilioni ya tani za nafaka. Lakini athari hizo huanzia katika maeneo kama Naporivske, ambako mkulima mmoja alirudi na kukuta ng'ombe waliokufa, mashamba yaliyokuwa yamejaa mabomu ya ardhini na mashine yaliyokuwa yameharibiwa vibaya-lakini akaamua kuanza upya.

European External Action Service published this content on August 27, 2026, and is solely responsible for the information contained herein. Distributed via Public Technologies (PUBT), unedited and unaltered, on August 31, 2026 at 13:08 UTC. If you believe the information included in the content is inaccurate or outdated and requires editing or removal, please contact us at [email protected]